Exodus 28:4-14

4 aHaya ndiyo mavazi watakayoshona: kifuko cha kifuani, kisibau, kanzu, joho lililorembwa, kilemba na mshipi. Mavazi haya yatashonwa kwa ajili ya ndugu yako Aroni na wanawe ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. 5 bWaambie watumie dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani safi.

Kisibau

6 c“Tengeneza kisibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kazi ya fundi stadi. 7Kitakuwa na vipande viwili vya mabegani vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kufungia kisibau. 8 dMshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi utafanana nacho: utakuwa kitu kimoja na hicho kisibau, nao utengenezwe kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri.

9 e“Chukua vito viwili vya shohamu, na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli 10kufuatana na walivyozaliwa: majina sita katika kito kimoja, na mengine sita katika kito kingine. 11Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya vito hivyo viwili kama vile sonara anavyochonga muhuri. Kisha uvitie vito hivyo katika vijalizo vya dhahabu, 12 fna uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kisibau yawe kama vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli. Aroni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele za Bwana. 13Tengeneza vijalizo vya dhahabu 14na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba, na uifunge mikufu hiyo kwenye vijalizo.

Copyright information for SwhNEN